Mkono wa Baba yetu Dhidi ya Wafilisti
5 1Wafilisti walikuwa wamelinyakua sanduku la Baba yetu, wakalileta kutoka Ebenezeri mpaka Ashdodi. 2Wafilisti wakalitwaa sanduku la Baba yetu, wakaliingiza ndani ya hekalu la Dagoni, wakaliweka kando ya Dagoni. 3Watu wa Ashdodi walipoamka asubuhi na mapema siku iliyofuata, tazama, Dagoni alikuwa amelala kifudifudi juu ya nchi mbele ya sanduku la Baba yetu. Wakamtwaa Dagoni, wakamrudisha mahali pake. 4Walipoamka asubuhi na mapema siku iliyofuata, tazama, Dagoni alikuwa amelala tena kifudifudi juu ya nchi mbele ya sanduku la Baba yetu. Wakati huu kichwa chake na mikono yake yote miwili ilikuwa imekatika na kulala juu ya kizingiti; kiwiliwili chake tu ndicho kilichobaki. 5Kwa hiyo hata leo makuhani wa Dagoni na wote waingiao katika hekalu la Dagoni huko Ashdodi hawakanyagi kizingiti cha Dagoni. 6Mkono wa Baba yetu ukawa mzito juu ya watu wa Ashdodi. Akawaharibu na kuwapiga kwa majipu—Ashdodi na nchi zote zilizoizunguka. 7Watu wa Ashdodi walipoona haya, wakasema, "Sanduku la Mungu wa Israeli lisikae kwetu; kwa maana mkono wake ni mzito juu yetu na juu ya Dagoni mungu wetu." 8Basi wakawaita pamoja watawala wote wa Wafilisti, wakauliza, "Tulifanyeje sanduku la Mungu wa Israeli?" Wakajibu, "Sanduku la Mungu wa Israeli na lihamishiwe Gathi." Basi wakalihamishia sanduku la Mungu wa Israeli huko.
9Baada ya kulihamisha, mkono wa Baba yetu ukaupiga mji ule pia, ukaleta hofu kuu sana. Akawapiga watu wake, wadogo kwa wakubwa, na majipu yakawatokea. 10Kwa hiyo wakalipeleka sanduku la Baba yetu mpaka Ekroni. Lakini lilipofika, watu wa Ekroni wakalia, wakisema, "Wametuletea sanduku la Mungu wa Israeli ili kutuua sisi na watu wetu!"
11Basi wakawakusanya watawala wote wa Wafilisti, wakasema, "Liondoeni sanduku la Mungu wa Israeli; lirudi mahali pake, ili lisije likatuua sisi na watu wetu." Kwa maana hofu ya mauti ilikuwa imeushika mji wote; mkono wa Baba yetu ulikuwa mzito sana huko. 12Wale ambao hawakufa walipigwa kwa majipu, na kilio cha mji kwa msaada kikapanda mpaka mbinguni.