Baba yetu Awaokoa Israeli Kupitia Sauli
11 1Kisha Nahashi Mwamoni akapanda na kupiga kambi dhidi ya Yabesh-gileadi. Watu wote wa Yabeshi wakamwambia Nahashi, "Fanya agano nasi, nasi tutakutumikia."
2Nahashi Mwamoni akajibu, "Nitafanya agano hili nanyi: nikin'goa jicho la kuume la kila mmoja, na kuleta aibu juu ya Israeli wote."
3Wazee wa Yabeshi wakamwambia, "Tupe siku saba tuwatume wajumbe katika nchi yote ya Israeli. Kama hakuna atakayetuokoa, tutajisalimisha kwako." 4Wajumbe wakafika Gibea ya Sauli, wakawaambia watu yaliyotukia, na wote wakalia kwa sauti kuu.
5Wakati ule ule Sauli akaingia kutoka shambani, akiwa nyuma ya ng'ombe zake. Akauliza, "Watu wana nini? Kwa nini wanalia?" Basi wakamwambia habari za watu wa Yabeshi. 6Sauli aliposikia maneno hayo, Roho wa Baba yetu akamjilia kwa nguvu; hasira yake ikawaka sana. 7Akatwaa jozi ya ng'ombe, akawakata vipande vipande, akavipeleka katika nchi yote ya Israeli kwa mikono ya wajumbe, akisema, "Hivi ndivyo watakavyofanyiwa ng'ombe wa kila mtu asiyetoka kumfuata Sauli na Samweli." Ndipo hofu ya Baba yetu ikawaangukia watu, nao wakatoka kama mtu mmoja. 8Akawahesabu huko Bezeki: Waisraeli 300,000, na watu wa Yuda 30,000. 9Wakawaambia wale wajumbe waliokuja, "Waambieni watu wa Yabesh-gileadi: Kesho, wakati jua litakapokuwa kali, mtaokolewa." Wajumbe wakaenda wakawaambia watu wa Yabeshi, nao wakafurahi. 10Watu wa Yabeshi wakasema, "Kesho tutajisalimisha kwenu; tufanyieni lolote mnalotaka." 11Siku iliyofuata Sauli akawagawa watu katika vikosi vitatu. Wakati wa zamu ya asubuhi wakaingia kambini, wakawapiga Waamoni hata joto la mchana; wale waliosalia wakatawanyika hata hapakubaki wawili pamoja.
Ufalme Wafanywa Upya Mbele za Baba yetu
12Watu wakamwambia Samweli, "Ni nani aliyeuliza, 'Je, Sauli atatutawala?' Watoeni watu hao—tutawaua."
13Lakini Sauli akasema, "Hakuna atakayeuawa leo, kwa maana leo Baba yetu ameleta wokovu katika Israeli."
14Samweli akawaambia watu, "Njooni, twendeni Gilgali tukaufanye upya ufalme huko." 15Watu wote wakaenda Gilgali, wakamfanya Sauli mfalme huko mbele za Baba yetu. Huko wakatoa dhabihu za sadaka za amani mbele za Baba yetu, na Sauli na watu wote wa Israeli wakafurahi mno.