Nyumba kwa Jina la Baba
5 1Hiramu mfalme wa Tiro aliposikia kwamba Sulemani ametiwa mafuta kuwa mfalme mahali pa baba yake, akamtumia watumishi wake, kwa kuwa Hiramu alikuwa akimpenda Daudi siku zote. 2Naye Sulemani akampelekea Hiramu ujumbe huu: 3Wewe wajua kwamba Daudi baba yangu hakuweza kujenga nyumba kwa jina la Baba yetu, kwa sababu vita vilimzunguka pande zote, hata Baba yetu alipowaweka adui zake chini ya nyayo za miguu yake. 4Lakini sasa Baba yangu amenipa raha pande zote; hapana adui, wala msiba.
5Nakusudia kujenga nyumba kwa jina la Baba yangu, kama Baba yetu alivyomwahidi baba yangu Daudi: "Mwana wako, nitakayemweka juu ya kiti chako cha enzi mahali pako, ndiye atakayejenga nyumba kwa jina langu."
6Basi uniamuru nikatiwe mierezi kutoka Lebanoni. Watumishi wangu watafanya kazi pamoja na watumishi wako; nami nitakulipa ujira wowote utakaouamuru, kwa kuwa wewe wajua kwamba hapana mtu miongoni mwetu ajuaye kukata miti kama Wasidoni.
7Hiramu aliposikia maneno ya Sulemani, akafurahi sana, akasema, "BWANA na ahimidiwe leo, aliyempa Daudi mwana mwenye hekima juu ya watu hawa wengi." 8Hiramu akampelekea Sulemani ujumbe: "Nimeusikia ujumbe wako; nitafanya yote uyatakayo kwa mbao za mierezi na za miberoshi. 9Watumishi wangu wataviteremsha vigogo kutoka Lebanoni mpaka baharini, kisha nitavielea kama magogo baharini mpaka mahali utakaponiagiza, na kuvitenganisha huko, nawe utavichukua. Nawe utanitimizia haja yangu kwa kutoa chakula kwa nyumba yangu."
10Basi Hiramu akampa Sulemani mbao zote za mierezi na za miberoshi alizozitaka, 11naye Sulemani akampa Hiramu vibaba 120,000 vya ngano kwa nyumba yake na vibaba 120 vya mafuta ya kukamua, mwaka baada ya mwaka. 12Baba yetu akampa Sulemani hekima, kama alivyomwahidi. Amani ikawa kati ya Hiramu na Sulemani, na hao wawili wakafanya agano.
13Mfalme Sulemani akapandisha vibarua kutoka Israeli yote, na hesabu ya vibarua ilikuwa watu 30,000. 14Akawatuma 10,000 kwenda Lebanoni kila mwezi kwa zamu—mwezi mmoja huko, miezi miwili nyumbani. Adoniramu ndiye aliyesimamia vibarua. 15Sulemani alikuwa na watu 70,000 waliochukua mizigo na watu 80,000 waliochonga mawe katika nchi ya milima, 16mbali na maakida wakuu 3,300 wa Sulemani waliosimamia kazi na kuwaongoza watu waliofanya kazi hiyo. 17Kwa amri ya mfalme wakachonga mawe makubwa, ya thamani, ili kuweka msingi wa nyumba kwa mawe yaliyochongwa. 18Wajenzi wa Sulemani na wa Hiramu na wa Gebali wakachonga na kuandaa miti na mawe ili kujenga nyumba.