Agano la Baba yetu na Daudi
17 1Baada ya Daudi kukaa katika nyumba yake, alimwambia nabii Nathani, "Tazama, mimi ninakaa katika nyumba ya mierezi, lakini sanduku la agano la Baba yetu limekaa chini ya mapazia ya hema."
2Nathani akamjibu Daudi, "Fanya yote yaliyomo moyoni mwako, kwa maana Baba yetu yu pamoja nawe."
3Lakini usiku ule neno la Baba yetu likamjia Nathani:
4Nenda ukamwambie Daudi mtumishi wangu: "Baba yako asema hivi: Wewe si ndiwe utakayenijengea nyumba ya kukaa ndani yake." 5Sikukaa katika nyumba tangu siku niliyowapandisha Israeli hata leo—bali nimehama hema hata hema, maskani hata maskani.
6Kila mahali nilipohama pamoja na Israeli wote, je, nalinena neno lolote kwa mmoja wa waamuzi wa Israeli, niliowaamuru kuwachunga watu wangu, nikiuliza, 'Kwa nini hamkunijengea nyumba ya mierezi?'
7Basi mwambie mtumishi wangu Daudi: "Baba wa majeshi ya mbinguni asema hivi: Nilikuchukua kutoka malishoni, kutoka kufuata kondoo, ili uwe mtawala juu ya watu wangu Israeli. 8Nimekuwa pamoja nawe kila mahali ulipokwenda, nami nimewakatilia mbali adui zako wote mbele yako. Sasa nitalifanya jina lako kama jina la wale walio wakuu wa dunia. 9Nami nitawachagulia watu wangu Israeli mahali, na kuwapanda huko, ili wakae nyumbani mwao wenyewe, wasisumbuliwe tena kamwe. Wala watu waovu hawatawadhoofisha tena kama zamani, 10tangu siku niliyowaweka waamuzi juu ya watu wangu Israeli. Nami nitawatiisha adui zako wote. Zaidi ya hayo nakuambia: Baba yako atakujengea nyumba. 11Siku zako zitakapotimia ukaenda kukaa pamoja na baba zako, nitainua uzao wako baada yako, mmoja wa wana wako, nami nitausimamisha ufalme wake. 12Yeye ndiye atakayenijengea nyumba, nami nitakisimamisha kiti chake cha enzi milele. 13Mimi nitakuwa Baba yake; naye atakuwa mwanangu. Wala sitauondoa upendo wangu wa agano kwake, kama nilivyouondoa kwa yule aliyekutangulia. 14Nami nitamweka juu ya nyumba yangu na ufalme wangu milele; na kiti chake cha enzi kitakuwa imara milele."
15Nathani akamweleza Daudi maneno hayo yote na maono haya yote.
Daudi Aketi Mbele za Baba yetu kwa Mshangao
16Ndipo mfalme Daudi akaingia, akaketi mbele za Baba yetu, akasema, "Mimi ni nani, Baba yangu, na nyumba yangu ni nini, hata umenileta mpaka hapa? 17Na kana kwamba hili lilikuwa jambo dogo machoni pako, Baba yangu—umenena habari za nyumba ya mtumishi wako kwa wakati ujao wa mbali, nawe umeniangalia mimi kama aliye mkuu kuliko wanadamu wote, Baba yangu. 18Daudi aweza kukuambia nini zaidi kwa kumheshimu mtumishi wako? Kwa maana wewe wamjua mtumishi wako. 19Baba yangu, kwa ajili ya mtumishi wako na kwa moyo wako mwenyewe, umeyatenda mambo haya yote makuu, ukizifunua ahadi hizi zote kuu. 20Baba yangu, hakuna aliye kama wewe, wala hakuna Baba ila wewe, sawasawa na yote tuliyoyasikia kwa masikio yetu. 21Ni taifa gani lililo kama watu wako Israeli, taifa moja duniani ambalo Baba yetu alikwenda kuwakomboa wawe watu kwake mwenyewe, ukijifanyia jina kwa matendo makuu na ya kutisha, ukiwafukuza mataifa mbele ya watu wako, uliowakomboa kutoka Misri? 22Uliwafanya watu wako Israeli kuwa wako mwenyewe milele, nawe, Baba yangu, ukawa Baba yao. 23Sasa, Baba yangu, neno ulilolinena juu ya mtumishi wako na juu ya nyumba yake na lithibitike milele; ukafanye kama ulivyonena. 24Na lithibitike, na jina lako likue milele, hata isemekane, 'Baba wa majeshi ya mbinguni ndiye Baba yetu juu ya Israeli.' Na nyumba ya mtumishi wako Daudi ithibitike mbele zako. 25Kwa maana wewe, Baba yangu, umemfunulia mtumishi wako ya kuwa utamjengea nyumba—kwa hiyo mtumishi wako amepata ujasiri wa kuomba mbele zako. 26Sasa, Baba yangu, wewe ndiwe Baba yetu; umemwahidi mtumishi wako jambo hili jema. 27Sasa umependezwa kuibariki nyumba ya mtumishi wako, ili idumu mbele zako milele; kwa maana wewe, Baba yangu, umeibariki, nayo imebarikiwa milele."